Tuesday, August 16, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUTOKURIDHISHWA NA TAARIFA YA UCHUNGUZI NA MAAZIMIO YALIYOTOLEWA NA KIKAO CHA BARAZA KUU LA UVCCM LILILOKUTANA TAREHE 13-08-2016 MJINI DODOMA

Ndugu waandishi wa habari, Salaam Poleni na majukumu ya kila siku ya ujenzi wa taifa, Leo mimi James Mwakibinga nimewaita hapa nikiwa kada wa CCM na mwanachama wa UVCCM, kuelezea na kutoa tathmini yangu juu ya maazimio ya Baraza kuu la UVCCM lililokutana Dodoma wikiendi iliyopita tarehe 13/08/2016.
Nafanya hivi kwa sababu kabla ya baraza kukutana nilitoa tamko la kuwaomba wayashughulikie na kuyamaliza matatizo na changamoto sugu zinazoikabili jumuiya yetu.

Napenda kuchukua nafasi hii kiasi kuwapongeza kwa uthubutu walioonyesha na hatua waliopiga kwani jitihada zozote zile ni kitu katika matumaini. Lakini niseme wazi kabisa kuwa hazitoshi na haziridhishi hata kwa kiwango tulichotarajia sicho walichoazimia.
Kama mnakumbuka Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi tulimpokea Dar es salaam kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe na mkutano mkuu wa taifa wa chama cha mapinduzi na kuwa mwenyekiti, tangu kuchaguliwa kwake kwa kura zote za ndio, Mwenyekiti amefanya mikutano kadhaa na wanachama wa CCM na kuonesha dira ya CCM anayoitaka. Ili kwenda na dira ya mwenyekiti ambayo imedhihirika katika utendaji wake na dhamira yake, mwenyekiti alionyesha kuwa anafahamu na anatambua kuwa jumuiya ya vijana haijazitumia fursa na rasilimali zake ipasavyo. Alionyesha kutokupendezwa na mwenendo wa baadhi ya wanachama wabadhirifu na wafujaji wa mali za jumuiya, na hapa ndipo nilipopata msingi wa tamko nililolitoa mimi muda mchache baada ya mkutano wa mwenyekiti na wanachama kuwasisitiza wajumbe wa baraza kwenda na kuenzi fikra na dira ya mwenyekiti katika kufanya maamuzi na maazimio.

Ndugu wanahabari, Kilichofanyika Dodoma katika baraza kuu la UVCCM ni funika kombe mwanaharamu apite, Kwa mfano Maazimio juu ya sakata la uuzwaji wa shamba la jumuiya huko Iringa, baraza limeamua kuwasimamisha kazi, kuwafukuza kazi na kuwavua nyadhifa zao watendaji na viongozi baadhi wa sakata hilo, nawapongeza sana angalau kwa hatua stahiki zilizochukuliwa.
  Na kuna maeneo mengi ambayo baraza kuu halikuyagusa katika kikao hiko , mfano  hawakugusia vile viwanja Mia mbili vya Temeke na vimeuzwa kinyemela na Mwenyekiti wa baraza la wadhamini Ndg.Dkt.Emanuel Nchimbi  na vimebaki vinne, Katika Majengo Pacha Ya Uwekezaji Makao Makuu UVCCM Dar, ikiambatana na taarifa ya Mapato yake na Matumizi .
Mwenyekiti wa baraza la wadhamini Ndg.Nchimbi anasemwa semwa kupewa floor nzima pale katika mradi,kipindi katibu mkuu akiwa martine Shigela , kuna Mradi wa Uwekezaji wa Vibanda vya kinondoni. Kuna eneo la saba Saba Dodoma , watu wamepanga Uvccm Kwa elfu kumi na wanapangisha watu wengine Kwa laki tatu, Haya yapo nchi nzima, Mradi wa uwekezaji Darajani na Gymkhana huko Zanzibar una madudu yake humo. Baraza kuu lenyewe likaona lijadili shamba la Iringa tu.

Ndugu waandishi wa habari jambo la kushangaza sana, kwenye taarifa iliyotolewa na baraza kuu,kwanza hakuna sehemu yeyote iliyozungumzia ripoti ya uchunguzi iliyofanywa mwezi Disemba 2015 na ndugu Egla Mwamoto aliyekuwa kaimu Katibu wa Hamasa na Chipukizi. Katika ripoti hiyo yapo maeneo yamewataja na kuwahusisha baadhi ya viongozi wakuu wa jumuiya ya vijana, wakati ndg.Egla Mamoto akisubiri kikao cha Kamati ya utekelezaji hili aweze kuiwasilisha ripoti hiyo maalumu ijadiliwe ,kikao husika cha Kamati ya utekelezaji kilipowadia kilimjadili ndgu .Egla na akatenguliwa nafasi yake ya Kaimu Katibu Hamasa na chipukizi Taifa. Kwa mujibu wa kanuni ya umoja wa vijana Mwenyekiti wa Kamati ya utekelezaji taifa ni Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, hivyo basi sisi kama vijana wa CCM tulitegemea Mwenyekiti wetu wa vijana angeweza kuwa na shauku ya kuwajua wabadhirifu wa mali za jumuiya kwa kuipa nafasi ripoti ya Ndg.Egla Mamoto katika kikao chao cha kamati ya utekelezaji kuliko kusimamia kikao hicho kumvua madaraka msamaria mwema huyu Ndg.Egla Mamoto.

Pili, Imeundwa sasa kamati nyingine ya kuhakiki na kufuatilia mali za jumuiya nchi nzima kwa miezi miwili mpaka watakapokutana mwezi oktoba katika Baraza kuu, nielezee mashaka yangu makubwa kama muda utatosha,lakini pili inawahusisha baadhi ya wajumbe wale wale wa kamati ya utekelezaji ile ile iliyoshindwa kutimiza wajibu wake wa kwanza wa kusimamia mali za jumuiya ya umoja wa vijana.

Baada ya uchambuzi huo mdogo ndugu zangu wanahabari ninadiriki kusema na mtakubaliana nami kuwa ndani ya jumuiya ya umoja wa vijana kuna mtandao wa wezi, wabadhirifu na wafujaji wa rasilimali za jumuiya.

Vitendo hivi vinavyofanyika katika jumuiya yetu ya vijana na baadhi ya viongozi na watendaji ni UJANGILI! Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na baraza kuu siku ya jumapili iliyopita ni wazi kuwa mtandao huu wa ujangili dhidi ya nyara za UVCCM unaanzia kwenye baraza la wadhamini, kwa viongozi wakuu wa jumuiya ya umoja wa vijana, kamati ya utekelezaji na watendaji wa chama na jumuiya waliotajwa. Hivyo baraza kuu kuwachukulia hatua baadhi ya watendaji wao na viongozi wachache bado haitoshi maana wahusika ni zaidi ya hao.

Ningependa kwa unyekekevu wa hali ya juu nifikishe maombi yangu kwa Mwenyekiti wetu mpendwa na katibu mkuu wa chama waingilie kati jambo hili ili kunusuru michakatochakato na makamatikamati haya kuwa mengi na yanayoyumbisha na pengine kuficha sehemu ya ukweli.

Ndugu zangu wana habari, baada ya maelezo hayo sasa nitoe mapendekezo yangu ili kusaidia kudhibiti na kupata ukweli ambao utapelekea hatua stahiki ziweze kuchukuliwa na haki kutendeka na katika CCM mpya kama isemavyo dira ya mwenyekiti :-

1. Kuvunjwa baraza la wadhamini na Mwenyekiti wake Ndg.Emmanuel Nchimbi kuchunguzwa;

2. Kuvunjwa kwa kamati ya utekelezaji ya Jumuiya ya vijana na Mwenyekiti wake Ndg. Sadifa Juma kusimamishwa ili kupisha uchunguzi;

3. Kuvunjwa kamati iliyoundwa na Baraza Kuu kuhakiki, kufuatilia na kuripoti juu ya hali za mali za jumuiya;

4. Kuundwa kwa Tume huru yenye mamlaka ,uwezo na ujuzi wa kutekeleza jukumu hili kwa uhuru na weledi (Tume hii ihusishe maafisa wa chama, vyombo vya ulinzi na usalama yaani Polisi, Takukuru, Ofisi ya CAG).

Mwisho, Ndugu zangu Wanahabari nawashukuru sana kwa mwitikio wenu na ni matumaini yangu makubwa kuwa mtayafikisha kama yalivyo na ni imani yangu mapendekezo haya yatapokelewa kwenye Chama chetu cha Mapinduzi na yakifanyiwa kazi yatafanikisha kuangamiza mtandao huu wa MAJANGILI katika kuelekea kwenye CCM mpya ya Mwenyekiti wetu Mh.Dkt.John Pombe Magufuli.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki CCM!

Asanteni kwa kunisikiliza.

Imetolewa leo Jumanne tarehe 16/8/2016 na:-
James Rock Mwakibinga 0717-362313/0628-888886
    (Sauti ya Nyikani)

No comments:

Post a Comment