Sunday, August 7, 2016

YANGA IJIANGALIE KWA UMAKINI

NAWAPENDA CCM, namna wanavyoendesha mambo yao kwa kufuata taratibu bila chembe ya ujanja ujanja au uhuni.
CCM wanaweza kuzibadili mwelekeo pepo kali za kusi kwenda kasi kwa misingi ya utaratibu tu na ukabaki mdomo wazi, hapa ilikuwaje!
Rejea mchakato wa kumpata mgombea Urais wa chama chao mwaka jana, Edward Lowassa ndiye mgombea aliyekuwa anaungwa mkono na watu wengi.
Lakini ndani ya chama wana wosia, miiko, maadili na utaratibu wao, ambavyo vyote vilikuwa vinamtakaa Lowassa aliyekuwa anaungwa mkono na wengi.
Pamoja na Lowassa kujipanga haswa dhidi ya hila ambazo kwa uzoefu wake ndani ya chama alijua angefanyiwa ili kufanikisha mpango wa kumuengua, lakini mwisho wa siku alienguliwa.

Lakini alienguliwa ndani ya utaratibu na mwisho wa siku akawa hana pa kwenda zaidi ya kuhamia upinzani, akijiunga na CHADEMA.
Ni utaratibu tu na CCM ikafanikiwa kuvuka kipindi kigumu zaidi katika historia yake na sasa Rais Dk John Pombe Joseph Magufuli anakijenga upya chama.
Utaratibu ninaozungumzia hapa, ni utaratibu ambao unaonekana kuwashinda wengi kutokana na desturi ya kupenda njia za mkato.
Mimi ni muumini mkubwa wa mabadiliko ya kimfumo katika uendeshwaji wa klabu kongwe nchini, Simba na Yanga na nimeanza kupigia kelele hilo tangu miaka ya 1990 naandika kwenye gazeti ya Mfanyakazi, baadaye Mtanzania, Dimba, Bingwa, The African, Rai, Tanzania Daima na Sayari.
Nimewahi pia kuandikia magazeti ya The Guardian, Nipashe, Lete Raha na Zanzibar Leo.
Nataka mabadiliko ya mfumo wa uendeshwaji ndani ya Simba na Yanga lakini si katika njia za kihuni kihuni, bali kwa utaratibu wenye kueleweka.
Suala la mabadiliko ya kimfumo ndani ya klabu kongwe kama hizo si la watu kukurupushwa ndani ya wiki moja na kuitwa mkutanoni, kisha kuulizwa; “mnanikodisha timu? semeni ndiyo au hapa”.
Mtaniwia radhi, naomba niseme huo ni uhuni. Na ni uhuni katika kitu cha kihistoria, chenye historia kubwa katika nchi yetu.
Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliitumia klabu ya Yanga katika harakati za Uhuru wa Tanganyika.
Vikao vya TANU vilikuwa vikifanyika kwa siri pale Jangwani kupanga mikakati ya kuikomboa nchi hii kutoka kwa Wakoloni – lakini anatokea mtu anataja aichukue timu kama ananunua samaki gulioni.
Hatukatai mabadiliko, lakini si kwa njia za kihuni kihuni kama hizo ambazo Mwenyekiti wa Yanga Yussuf Manji anataka kutumia sasa.
Mkutano wa jana Diamond Jubilee, uliitishwa ndani ya wiki moja, jambo ambalo ni kinyume cha Katiba ya klabu.
Baraka Deusedit na Jerry Muro hata Uyanga wao ni wa juzi na bila shaka walipewa kadi za Yanga ili kuhalalisha utumishi wao ndani ya klabu. Hawa hawawezi hata kuwa na uchungu na klabu yenyewe.
Lakini vipi Francis Kifukwe, Isaac Chanji, Ibrahim Akilimali, Soud Tall, Thomas Mdeka, Tony Shebuka, Mohammed Bhinda, wote hawa ni Yanga wa siku nyingi na wanaijua historia ya klabu – kwa nini wanakubali kuiuza kama kitunguu gengeni?
Fedha. Kweli fedha zimetufikisha kwenye kuisaliti klabu. Kifukwe anasimama mbele ya Mkutano wa hadhara anaridhia klabu kukodishwa katika mazingira ya kihuni.
Wanachama watatu waliofukuzwa jana, Salum Mkemi, Hashim Abdallah na Ayoub Nyenzi kosa lao ni nini? Wanachama wa Yanga waliafiki waondolewe, lakini hawajajua kosa lao ni nini.
Tu Mwenyekiti kasimama kasema; “Mimi siwezi kufanya kazi na hawa watu”. Basi kazi ipo, kama hata Rais Magufuli angekuwa anafanya hivyo sijui ingekuwaje.
Mtu ambaye anasimama anasema Yanga inaonewa imeshinda Kombe la TFF na Ligi Kuu lakini haipewi fursa ya kucheza Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho kwa pamoja. 
Huyo ni mtu ambaye hajui kwamba hata Ulaya Barcelona inashinda mataji yote ya Hispania, lakini huwezi kuikuta inashiriki Ligi ya Mabingwa na Europa League.
Na hajui pia kwamba hata DRC, TP Mazembe inashinda mataji yote, lakini huwezi kuikuta inacheza Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa. Huyo mtu maana yake hajui mpira na ni mtu ambaye anahitaji kufundishwa kwanza – lakini ajabu huyo ndiye mtu anayewaburuza watu waliozaliwa kwenye mpira na wenye Masters na PhD za Marekani na Ukaya.   
Hapa wanatazamana vipi? Wanasalitiana wana Yanga kwa wana Yanga na nafsi zao zinajua. Sura zao zimejaa unafikia, halafu wanawaita wengine wanafiki. Nani mwenye uchungu na Yanga kama wale tunaoamini ni wana Yanga wazuri waliopewa dhamana kubwa sasa wanaisaliti klabu. Na si kusema wana njaa, wengine ni ulafi tu!



imehamishwa toka Bongostaz

No comments:

Post a Comment