Monday, August 1, 2016

MO AWASILISHA BARUA RASMI SIMBA SC


Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
BILIONEA namba 21 Afrika, Mohamed Gulam Dewji amewasilisha barua rasmi ya kutaka kuinunua klabu ya Simba ya Dar es Salaam.
Na hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Mkutano Mkuu wa mwaka wa Simba SC jana kuridhia mabadiliko kwa kuingia kwenye mfumo wa kuuza hisa.
Mo Dewji, tajiri namba moja kijana Afrika kwa mujibu wa jarida la Forbes la Marekani, ameyasema hayo asubuhi ya leo katika Mkutano na Waandishi wa Habari, jengo la Godlen jubilee Towers, Mtaa wa Ohio, Dar es Salaam.  
“Leo asubuhi kitu cha kwanza nimefanya ni kuandika barua na kuipeleka ofisini kwa Rais wa Simba, Evans Aveva. Na nimefika nimekuta ofisi yake haijafunguliwa, ikifunguliwa ataikuta barua ya kwanza ni yangu pale,”amesema Mo Dewji.
 Mo Dewji akizungumza na Waandishi wa Habari leo ofisini kwake


Mo amesema katika barua hityo ameandika kwamba yeye ni mwanachama aliyewahi kuwa mfadhili wa timu, ambaye sasa anataka awekeze Sh. Bilioni 20 kwa kununua asilimia 51 ya hisa za klabu.
“Nimesema fedha hizo zitawekwa kwenye akaunti maalum na hazitaguswa. Nataka mchakato huu utimie ndani ya miezi mitatu kama inawezekana,”amesema. 
Hata hivyo, Mo amesema anasikitika baadhi ya viongozi wa Simba chini ya rais Aveva wanaonekana hawataki mabadiliko.
“Jana nilikuwa nafuatilia mkutano, nilisikia hoja kadhaa kwa namna moja au nyingine, ziliniumiza na zilikuwa za upotoshaji. Wanasema natangaza kwenye vyombo vya habari tu, hatujawahi kukutana. Leo niwe muwazi zaidi, nimekwishakutana na Aveva zaidi ya mara tatu. Na amewahi kuja ofsni kwangu zaidi ya mara tatu. Alikuja na (Geoffrey Nyange) Kaburu (Makamu wa Rais).  Hizi dhana tunamsikia Mo kwenye vyombo vya habari si za kweli,”. 
“Lakini pia, kulikuwa kuna hoja Mo anasema kwa maneno si kwa maandishi, sisi tulikuwa tunangojea wanachama waridhie mabadiliko ya mfumo, kwa kuwa wameridhia na ninawashukuru sana. 
Leo asubuhi kitu cha kwanza nimefanya ni kuandika barua na kuipeleka ofisini kwa Rais wa Simba, Evans Aveva,”amesema na kuongeza. “Sasa barua kapata, nitamuomba Evans ajaribu kukaa na Kamati ya Utendaji, ili waone namna ya kufanikisha hili jambo haraka,”aliongeza Dewji.
Aidha, Dewji alisema ahadi yake ya kusaidia usajili wa wachezaji Simba SC wakikubali mabadiliko iko pale pale. “Ahadi yangu iko pale pale, lakini lazima viongozi waridhie,”alisema.
Katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa Simba SC uliofanyika jana, uongozi uliridhia ombi la wanachama kutaka mabadiliko na kuingia kwenye mchakato huo mara moja.
Na wanachama walishinikzia mabadiliko baada ya Mo Dewji kutangaza ofa ya kununua asilimia 51 ya hisa za klabu kwa Sh. Bilioni 20 na kuwekeza.
Na Mo ameahidi kuifanya Simba iwe klabu bora zaidi nchini iwapo atafanikiwa kupewa hisa.  

No comments:

Post a Comment