Na Samuel Samuel
Awali ya yote ningeomba tuitambue kwa ufupi sana klabu hii ya Young Africans ‘Yanga’ tangu ilipoanzishwa, maendeleo iliyofikia , mifumo ya uendeshaji toka kuanzishwa kwake na mustakabali wake kabla ya hili.
Young Africans Sports Club al maarufu kama timu ya wananchi, ilianzishwa mwezi Februari tarehe 11 mwaka 1935 ikiwa timu kongwe zaidi Tanzania kwa umri wa miaka 81.
Klabu hiyo yenye masikani yake mitaa ya Twiga na Jangwani viunga vya Kariakoo, moja ya rasimali zake kubwa ni rasilimali watu. Inakadiriwa kuwa na mashabiki zaidi ya milioni 8 nchi nzima ikiwa na takribani ya matawi makubwa zaidi ya 20 nchi nzima yenye wanachama hai zaidi ya 500 kwa kila tawi.
Young Africans katika kipindi cha miaka yote hiyo 81 kwa upande wa maendeleo ya klabu iliyapata zaidi miaka ya 70 (1972) kwa kujenga makao makuu yake pale Jangwani na uwanja wa mazoezi wa Kaunda upenuni tu mwajengo la makao makuu. Ujenzi uliofanywa na Kampuni ya Mecco kwa msaada mkubwa wa hayati Abeid Karume aliyekuwa raisi wa kwanza wa Zanzibar.
Hali hii ilifanya klabu hiyo kujiongezea mashabiki na wanachama lukuki pia ikifanya vyema kwenye ligi ya ndani na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kujichukulia vikombe kadhaa.
Wakati wote huo klabu hiyo imekuwa ikiendeshwa kwa hisani za wafadhili na wadhamini ikiwa katika mfumo wa kumilikiwa na wanachama wa klabu hiyo.
Baada ya maendeleo hayo ya miaka ya 70, klabu hiyo imeshindwa kupiga hatua zaidi katika kujitanua kiuchumi na kuendelea kuishi kwa hisani za wafadhili na wadhamini.
Naweza sema katika mfumo huo klabu hii imeendelea kujiongeza katika rasilimali watu lakini pasipokuwa na maendeleo yoyote ya maana kwa maana ya klabu kupata misuli bora ya uchumi kama zilivyo klabu kongwe Afrika zenye umri sawa na klabu hiyo mfano TP Mazembe, Al Ahly na Zamaleki.
Wafadhili na viongozi wengi waliopita wametumia nguvu kubwa kuwekeza kwenye timu na si klabu nzima kwa ujumla ndio maana Young Africans imeendelea kuwa bora kimbinu na kiufundi ndani ya dakika 90 lakini si kwa miundo mbinu bora kwa kutumia brand yake kujitanua kiuchumi.
Yusufu Manji ambaye amekuwa na klabu hii kwa takribani miaka kumi , alianzakuwa mfadhili wa klabu hii akisaidia uendeshaji wa timu kwa mamilioni ya pesa katika usajili wa wachezaji , makocha pia kuigharamikia timu kiutawala kwa ujumla.
Manji baada ya kugundua mfumo wa kusimama kama mfadhili halitimii lengo sahihi la kuifanya timu hiyo kusimama imara kwa wingi wa wanachama na viongozi walafi kuchakachua sehemu ya ufadhili wake , aliamua kugombea nafasi ya uenyekiti ili kupitia falsafa zake za uongozi aweze kuisimamia vyema timu hiyo na kusonga mbele.
Wahenga wanasema “hakuna hisani isiyo na malengo”
Manji amekuwa na ndoto za kuifanya klabu hii iinuke vyema idara zote upande wa timu na maendeleo ya klabu kiuchumi. Hii ina maana ifike wakati klabu ijiendeshe kwa uchumi wake kutokana na thamani kubwa ya brand ya klabu hiyo.
Leo niliposikia anaitaka timu hii kwa asilimia 75 akiwaachia asilimia 25 wanachama , hakika hili nililitegemea siku nyingi. Tofauti limekuja kwa njia tofauti. Halijaja katika mfumo wa hisa.
Imefika wakati kuiongozi huyo ambaye amekuwa akiihudumia klabu hiyo kwa zaidi ya asilimia 90 ameamua kuifanya klabu hiyo kuwa sehemu ya makampuni yake ya Quality Group ili kuzipa thamani pesa zake ambazo kwa hakika hazikuwa zinaleta mrejesho chanya kwa asilimia 100.
Nini maana ya umiliki huu au ni mfumo gani?!
Simba SC ina mchakato wa kuingia kwenye mfumo wa kujiendesha kwa hisa kwa asilimia 100 hii ina maana klabu hiyo inaua kabisa mfumo wa kumilikiwa na wanachama wake ambao wameilea timu hiyo kwa miaka 80. Wanageuka mashabiki kwa asilimia 100 na kuiacha klabu yao kumilikiwa na yoyote yule mwenye uwezo wa kununua hisa.
Manji ameomba kuimiliki Yanga SC kwa asilimia 75 katika brand yake. Yaani ameomba kumiliki mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo kwa asilimia 75 na asilimia 25 akiziacha kwa wamiliki wa timu hiyo ambao ni wanachama.
Hizi asilimia 25 ni mali zisizo hamishika za klabu yaani majengo na uwanja wa Kaunda.
Kwa miaka 81 maendeleo yalifikiwa mwaka 1972 tu kwa hisani ya mzee Karume na baadhi ya wanachama lakini toka hapo hakuna lolote la maana hivyo kujitokeza mtu huyu ambaye anahitaji kuiendesha klabu hiyo kwa faida kwa asilimia 75 si jambo la kupinga hata kidogo.
Kikubwa ningeomba bodi ya ligi na wanachama waandamizi wa klabu hiyo wautafakari kwa kina mchakato huo na uboreshwe kwa kuwapa mamlaka wanachama ndani ya miaka hiyo 10 wawe na mamlaka ya kutengua mkataba huo endapo yaliyozungumziwa katika nusu ya kwanza kwa maama ya miaka 5 ya awali yasipofikiwa.
Imezungumzwa asilimia 25 ambazo wanachama watabaki nazo ndizo zitatumika kuboresha majengo na uwanja wa Kaunda. Ni vyema kabla ya mchakato kufikiwa wanachama na bodi ya wadhamini ya klabu hii waangalie tafsiri sahihi ya umiliki wa asilimia 75 wa brand ya timu ili klabu hata baada ya miaka 10 ya mkataba huu iwe imejiongeza katika miundombinu mipya ya kiuchumi.
Mwisho kabisa niseme jambo moja, mpira ni pesa na wanapotokea wawekezaji kama hawa ambao wameamua kuiendesha klabu kwa faida pande zote yaani kwao na klabu basi hatamu yenye tija itafikiwa kwa maana hawatakubali hasara kwa uwekezaji mkubwa watakao weka.
No comments:
Post a Comment