Tuesday, August 30, 2016

TFF YAGHAIRISHA TENA LIGI KUU TANZANIA BARA

Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imethibitisha kuwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Young Africans ya Dar es Salaam na JKT Ruvu ya Pwani, ulipangwa kufanyika Jumatano Agosti 31, 2016 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam imeahirishwa mpaka itakapopangiwa tarehe nyingine.

Mechi hiyo imeondolewa kutokana na timu ya Young Africans kuwa na wachezaji wengi kwenye kikosi cha timu ya Taifa (Taifa Stars) kinachosafiri Agosti 31, 2016 asubuhi kwenda Lagos, Nigeria kwa ajili ya mechi ya mchujo ya michuano ya Kombe la Afrika (AFCON Qualifiers) itakayochezwa Septemba 3, 2016.


Mabadiliko hayo hayatavuruga ratiba ya mechi zinazofuata za Ligi Kuu ya Vodacom kwa timu husika. 

Pamoja na taarifa hiyo ya TFF, inaonekana ni kilekile kichekesho cha kuanza kupanguliwa kwa ratiba mapema zaidi.

Kwani TFF na Bodi ya Ligi wakati wakipanga ratiba, walikuwa wanajua kabisa mechi hiyo itakuwepo na Yanga wana uwezekano mkubwa wa kuwa na wachezaji wengi.

TFF ilikuwa inajua lazima timu itasafiri kwenda Nigeria kumalizia mechi hiyo ambayo unaweza kuita ya kusaka heshima au kujifurahisha.

Lakini Yanga ambayo imechelewa kuanza ligi kutokana na majukumu ya kimataifa, sasa mechi yake nyingine inaahirishwa na inaonyesha kuwa dalili za mambo kwenda hovyohovyo msimu huu, imeanza mapema.

Kwani wakati timu ndiyo zinacheza mechi za pili, tayari ratiba inabadilishwa au inafanyiwa mabadiliko mara mbili.

Wakati Yanga ndiyo imecheza mara moja, ratiba inayoihusu ya ligi, imeanza kutundikiwa viraka.

No comments:

Post a Comment