Friday, August 26, 2016

WABUNGE MASHABIKI WA SIMBA WABARIKI MCHAKATO WA MO

WABUNGE ambao ni mashabiki wa timu ya Simba wametoa baraka kwa mchakato wa uwekezaji ndani ya klabu hiyo unaotaka kufanywa na mfanyabiashara Mohammed Dewji 'Mo'.

Wabunge hao walikutana leo mjini Dodoma kuzungumzia mustakabali wa klabu hiyo ikiwemo mchakato wa uwekezaji ambao Mo ameridhia kununua hisa 51% kwa sh 20 bilioni ambazo zitatumika kujenga uwanja, hostel, gym pamoja na miundombinu mingine ya timu hiyo.

Mbunge wa jimbo la Chemba Juma Nkamia alisema wameungana na Wanasimba wote kupongeza mchakato wa uendeshwaji wa klabu ambapo wanachama wataruhusiwa kununua hisa.

"Tulikuwa na kikao cha wabunge mashabiki wa  Simba na kwa pamoja tumebariki mabadiliko ambayo yanatarajiwa kutokea ndani ya klabu yetu kuhusu uwekezaji," alisema Nkamia.

Nkamia aliwahi kuwa Katibu Mwenezi wa timu ya Simba miaka ya nyuma na kujitahidi kuipigania klabu hiyo wakati akiwa mtangazaji wa shirika la utangazaji Tanzania TBC.

Julai 31 mwaka huu wanachama wa klabu ya Simba walipitisha mabadiliko ya uendeshwaji kwa kuingia katika mfumo wa hisa ambao Mo amejitokeza kuwekeza mabilioni hayo.

Wiki mbili zilizopita kamati ya utendaji ya klabu ya Simba ilikutana na Mo kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo likamilike mapema.

No comments:

Post a Comment