By Dick Dauda -
October 21, 2016
Kocha mkuu wa Simba Joseph Omog ameandika rekodi mpya ndani ya klabu ya Simba msimu huu baada ya kucheza mechi 10 bila kupoteza. Ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Mbao FC kwenye uwanja wa Uhuru, ulikuwa ni ushindi wa nane tangu kuanza kwa msimu huu huku ukiwa ni ushindi wa tatu mfululizo.
Rekodi zinasemaje?
Msimu wa 2009-2010 Patrick Phiri alioongoza Simba kutwaa taji la ligi kuu Tanzania bara bila kupoteza mechi hata moja.
Abdallah Kibadeni ‘King Kibadeni’ akisaidiana na Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ ndiyo makocha wengine walioisaidia Simba kucheza mechi 10 za mwanzo wa ligi bila kupoteza mchezo katika msimu wa 2013-14.
Katika mechi hizo 10 zilizosimamiwa na Kibadeni pamoja na Julio, Simba ilifanikiwa kushinda mechi 5 huku mechi 5 nyingine ikitoka sare. Katika msimu huo, Simba ilipoteza mechi yake kwa mara ya kwanza dhidi ya Azam FC kwa kipigo cha magoli 2-0 msimu ambao pia Azam walitwaa taji la gili mwishoni mwa msimu.
Rekodi aliyoweka Omog
Mcameroon huyo amefanikiwa kuiongoza Simba kushinda mechi nane na kutoka sare mara mbili katika mechi 10 za kwanza tangu kuanzanza kwa msimu huku Simba ikiwa ni timu pekee ambayo bado haijaonja ladha ya kipigo hadi sasa. Licha ya kuwa sawa na King Kibadeni kwa kuiongoza Simba katika mechi 10 bila kupoteza, Omog anabebwa na idadi ya mechi ambazo Simba imepata ushindi.
Simba ikiwa chini ya Omog imeshinda mechi 8 na kutoka sare katika mechi mbili wakati wa Kibadeni Simba ilishinda mechi 5 na kutoka sare katika mechi 5 katika mechi 10 za mwanzoni mwa ligi wakisimama kama wakufunzi wakuu wa klabu hiyo ya mtaa wa Msimbazi.
Je yatajirudia ya msimu wa 2013-14?
Licha ya Simba kuanza vizuri msimu huo, haikufanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi badala yake ikamaliza ligi ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo huku Azam wakitwaa taji hilo kwa mara ya kwanza chini ya Omog aliyerithi mikoba ya Stewart Hall Desemba 2013.
Kwa sasa Simba ipo inaongoza ligi ikiwa chini ya Omog kwa pointi zake 26 baada ya kucheza mechi 10. Omog aliisaidia Azam kutwaa taji la kwanza katika historia yao msimu wa 2013-14. Je msimu huu ataisaidia Simba kutwaa taji la kwanza baada ya kupita kavu katika misimu mitano?
Kutimuliwa
Mwishoni mwa msimu wa 2013-14, King Kibadeni na Julio walifutwa kazi na uongozi wa klabu ya Simba kutokana na klabu hiyo kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi na nafasi hiyo kuchukuliwa na Zdravco Lugarusic.
Licha ya kuwapa ubingwa kwa mara ya kwanza katika historia yao, Azam walimtimua Omog mwaka 2015baada ya kipigo cha magoli 3-0 ugenini na klabu ya El Merreikh ambacho kilipelekea Azam kutupwa nje kwenye ligi ya mabingwa Afrika katika hatua ya awali
No comments:
Post a Comment