Sheila Ally, Mbeya
NYOTA wa Simba, Laudit Mavugo jana alikaa benchi kwa dakika zote 90 akiwaangalia wenzake wanavyopambana kwenye uwanja wa Sokoine dhidi ya Mbeya City na Jackson Mayanja ambaye ni kocha msaidizi ametamka kuwa Simba ni ya wote hivyo watu wasiwe na imani potofu mchezaji anapokaa benchi.
Mayanja aliyazungumza hayo mara baada ya mechi hiyo waliyoshinda bao 2-0 kwamba kitu pekee kilichopo ndani ya Simba kwasasa ni umoja na mshikamano huku akiamini kwamba kila mchezaji ndani ya Simba ana uwezo mkubwa wa kucheza kwa mafanikio.
Mayanja alisema kuwa mechi bado nyingi ambapo wachezaji wote watacheza na si kwamba wanaokaa kwenye benchi uwezo wao umeshuka ila hayo ni mabadiliko ambayo kila mmoja anapaswa kuyaelewa.
"Hata huyo Juuko ana uwezo mkubwa ila watu watofautishe kati ya ngazi ya Taifa na ngazi ya klabu, kwenye klabu ni kugumu kuliko timu ya Taifa hivyo muda utafika hata huku atacheza tu ndio maana nasema Simba ni ya watu wote kila mchezaji anapaswa kuichezea," alisema Mayanja.
Akizungumzia zaidi mechi hiyo alisema kuwa Mbeya City ni timu nzuri ingawa imeshindwa kupata matokeo mazuri huku akifafanua kuwa wao walijiandaa vyema na ndiyo maana wakashinda.
"Ukijipanga vizuri lazima upate matokeo mazuri sisi tulijipanga kuliko Mbeya City, nawapongeza vijana wangu wamecheza kwa kujitolea maana kucheza ugenini ni kugumu, lengo letu tunataka kumaliza mzunguko wa kwanza tukiwa juu kabisa nikiwa na maana kwamba tunataka kufunga hesabu mapema," alisema Mayanja.
Kwa upande wa Mbeya City, kocha Kinnah Phiri alisema kuwa; ,"Tumejitahidi kucheza lakini hatukuwa na bahati na wachezaji wangu walishindwa kutumia nafasi walizopata kama ilivyokuwa kwa wapinzani wetu walipata nafasi wakazitumia vizuri."
No comments:
Post a Comment