Saturday, August 20, 2016

ASANTE SANA MUSSA HASSAN MGOSI


Na Oscar Oscar

Maisha ya Soka ni  ya muda mfupi sana, kwa bahati mbaya wachezaji wengi hawalijui. Wanadhani kwamba kila siku wataendelea kupiga pesa, kila siku wataendelea kuhama kutoka klabu moja kwenda nyingine. Maisha ya wachezaji yanahitaji mahesabu sana, ndiyo maana mpaka leo Nwanko Kanu anaendelea kuingiza Pesa wakati  amestaafu soka miaka kibao iliyopita. Mshambuliaji wa Simba, Mussa Hassan Mgosi ametangaza kustaafu Soka rasmi na mechi kati ya Simba dhidi URA ya hivi karibuni ndiyo ilikuwa wa mwisho kwa mkongwe huyo. Umejiandaa vizuri Mgosi?

Wachezaji wengi wa Kitanzania wamekuwa wakijisahau sana kuandaa maisha yao nje ya Uwanja. Muda mchache baada ya kustaafu soka, hugeuka omba omba. Kuna haja ya wachezaji wetu kupewa elemu ya namna ya kuishi baada ya kustaafu. Tumekuwa na orodha ndefu sana ya wachezaji wakongwe wakionekana kupata tabu sana hasa pale wanapokuwa wagonjwa. Wengi husikika kwenye vyombo mbalimbali vya Habari wakiomba msaada kwa wadau ili wapate matibabu, kiuhalisia mambo haya yanawakuta ndugu zetu kwa sababu tu ya kutojiandaa mapema. Asante Mussa Hassan Mgosi kwa kutuburudisha sisi mashabiki wa mchezo wa Soka lakini, umejiandaa vema kwenye maisha baada ya kustaafu?

Wachezaji wengi wamekuwa na tabia ya kuishi maisha ya kifahari sana wakati wanapokuwa kwenye kiwango bora kiasi cha kujisahau. Tumekuwa na watu ambao hawakumbuki maishi yao ya baadae, wachezaji wengi wamekuwa na maisha kama Popo kila Siku ni kujirusha tu. Huwa napata wakati mgumu sana ninaposikia mchezaji wa Kibongo anatangaza kuachana na Soka kwa sababu umekuwa ni mwanzo wa wao kugeuka ombaomba. Asante sana Mgosi kwa kucheza Soka kwa zaidi ya miaka 10 Sasa lakaini umejiandaa vizuri na maisha nje ya dimba?

Kuna muda klabu za Simba na Yanga zimekuwa zikipewa lawama sana kutokana na kutowahudumia wachezaji wao wa zamani hususani pale wanapopatwa na matatizo lakini kwa kufanya hivyo kiuhalisia ni kuwaonea bure. Hawa wachezaji wakati wakicheza hulipwa mishahara, posho na pesa za usajili. Kutokana na kutokuwa na mahesabau mazuri ya maisha yao ya baadaye, hutumbua Pesa zote na matokeo yake muda mfupi baada ya kustaafu hujikuta wakiishi maisha magumu sana. Mgosi umejipanga sawa sawa kwa maisha  ya nje ya Uwanja?

Wachezaji wetu wanapaswa kupewa elemu juu ya mifuko mbalimbali ya kijamii na bima za afya. Wanapaswa kufundishwa ujasiliamali na namna ya kujiwekea akiba ili wanapostaafu wasiweze kuwa ombaomba kwa muda mfupi. Moja kati ya washambuliaji bora wazawa kwa miaka 10 ya hivi karibuni ni pamoja na Mussa Hassan Mgosi lakini itasikitisha kumuona baada ya muda mfupi tangu kustaafu Soka akionekana ombaomba. Itakuwa ni jambo la kusikitisha kama Mgosi bado ataendelea kucheza mechi za mchangani ili angalau apate Pesa ya kujikimu. Wachezaji wetu wanapokuwa juu hujikuta wamekuwa walevi wa kutupwa, starehe mwanzo mwisho Waikati maisha ya Soka ni muda mfupi sana. Unapaswa kutengeneza Pesa ndani ya miaka 10, utakayoitumia kwa maisha yako yote. Kuna haja kubwa sana ya wachezaji wetu kufundishwa shughuli mbalimbali za kujiongezea kipato wakati bado wakiwa na nguvu za kucheza Soka ili wanapostaafu wasipate tabu Sana. Nakupongeza Mgosi kwa kuipigania Simba, Mtibwa Sugar na Taifa Stars kwa zaidi ya miaka 10 lakini umejiandaa vizuri kwa maisha baada ya Soka?

Umefika wakati tuone aibu kila siku wachezaji wetu wa zamani kugeuka ombaomba wakati Enzi zao walikuwa walevi wakutupwa. Wanapaswa kuambiwa ukweli juu ya mustakabali wa maisha yao. Kila mtu anapaswa kuubeba msalaba wake wenyewe. Kila tasinia imekuwa na wakongwe wake, mbona kwenye Soka ndiyo kumejaa ombaomba? Kila mtu anajukumu la kuandaa maisha yake ya Sasa na ya baadae. Ifike wakati wachezaji wetu wajue umuhimu wa kujiwekea akiba. Habari za kula ujana kwa kishindo kisha unakuja kusumbua watu uzeeni hatuna budi kuzikataa. Pengine wachezaji wa Soka wanadhani kwamba umaarufu wao ndiyo akiba ya uzeeni, wanasahau kwamba kila zama zina mfalme wake. Muda wako ukimalizika kwenye Soka unakwenda nje na mwingine anaibuka. Tabia ya kugeuka ombaomba inabidi ikomeshwe ili kuwafanya wachezaji wetu kuwa na nidhamu ya Pesa pindi wanapokuwa wanalipwa Pesa nyingi. Najiona mwenye bahati kupata nafasi ya kumshuhudia Mussa Hassan Mgosi akiwa ndani ya jezi ya Simba lakini nitakuwa mwenye bahati zaidi endapo sitikuja kumshuhudia Mgosi akigeuka ombaomba. Amepata nafasi ya kucheza Soka ndani na nje ya nchi tena kwa muda mrefu, naamini ametengeneza Pesa ndefu na amejipanga kikamilifu kufurahia maisha take nje ya Soka.

Kuendelea kuwasaidia wachezaji wetu wakongwe kila wanapopata Shida bila kutoa elimu kwa hawa wanaocheza Leo, nikuendelea kuzalisha ombaomba wengine. Tunahitaji kuwasaidia hao ambao bado wananguvu ili kuwajengea maisha ya baadae. Wengi wanaanza Soka wakati akili bado hazijakomaa vizuri na matokeo yake ujana, Pesa na umaarufu wanashindwa kuvimudu na kujikuta wakiharibu maisha yao ya baadae. Nakushuru sana Mussa Hassan Mgosi, naamini umejipanga sawasawa kwa maisha yako mapya. Nakutakia kila la kheri, asante kwa kutupa burudani.

No comments:

Post a Comment