Tayari Yanga kupitia Baraza la Udhamini ilisaini mkataba wa ukodishwaji wa timu, nembo na jengo kwa miaka kumi na Kampuni ya Yanga Yetu Limited, ambapo kauli ya BMT imekuja ikiwa tayari Yanga wamekubali kukodisha mali zake.
BMT imetaja mambo matano ambayo klabu hizo zinapaswa kuyazingia ambayo ni kutumia vikao mbalimbali ndani ya klabu zao vilivyowekwa kwa mujibu wa katiba zao. Kikao cha kwanza ni kamati ya utendaji ya klabu. Kamati ambayo itajadili jambo linalokusudiwa kwa kina, kwa kuchambua faida na hasara ya jambo lenyewe.
Na wakikubaliana kukubaliana au wakikubaliana kutokukubaliana, muhtasari uandikwe ili upelekwe kwenye kikao cha juu cha klabu husika. Taratibu za kuitisha kamati ya utendaji zipo kwenye Katiba ya kila klabu na dosari yoyote ikianzia hapa basi zoezi zima litakuwa batili.
Pili, Mkutano Mkuu wa wanachama wote, aidha uwe wa dharula au wa kawaida, uitishwe na maelekezo ya namna ya kuitisha, kujadiliana na kufikia maamuzi yapo wazi kwenye katiba za klabu. Ni Haki ya msingi ya wanachama kupewa taarifa, kuijadili na pengine kuomba ushauri wa kitaalamu au wa kiufafanuzi wapewe pasipo na shaka ili waelewe vizuri, watakapotoa maamuzi yasiwe na mashaka juu ya haki zao za kikatiba.
Tatu, Baraza la wadhamini lenye uwezo wa kuingia katika maamuzi makubwa kama haya ni lazima lenyewe liwe lile lililopitishwa na mkutano mkuu na wala lisiwe la muda. (Baraza la wadhamini la muda). Ikumbukwe kuwa maamuzi haya sio madogo ni maamuzi yanayoweza kusababisha fujo, vurugu, kutokubaliana kwa lolote kutasababisha upotevu/uvunjifu wa amani si michezo pekee bali nchi kwa ujumla wake.
Nne, Baada ya taratibu hizo zote kufuatwa muhtasari utaandikwa na kupelekwa kwa msajili ili kwa mujibu wa sheria ya Baraza ya mwaka 1967 – Kifungu namba 11 (1) kinaeleza 'Chama chochote kinachofanya mabadiliko ya jina, anuani, madhumuni au kifungu chochocte cha katiba yake kitatakiwa kupata idhini ya msajili kwa kupeleka maombi kwa msajili kupitia Msajili Msaidizi'.
Kifungu namba 11 (3) Msajili kuyakataa maombi ya kubadili kifungu chochote cha katiba ya chama kama:-
a. Ataona kuwa mabadiliko yanaweza kuhatarisha usalama na kuvuruga amani miongoni mwa wanachama na jamii kwa ujumla hivyo kuathiri maendeleo ya chama.
b.Msajili atabaini kuwa malengo hayo yanalenga kuwanufaisha wachache.
d.Kama anaona kuwa mabadiliko hayazingatii Sera ya michezo na Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa. Msajili ndiyo atatoa maamuzi ya kukubali au kukataa kadri atakavyoona jambo lenyewe kama lina maslahi kwa nchi au halina.
Mwisho baada ya hatua zote hizo kukamilika, inabidi kufanya marekebisho ya Katiba ambayo yatapitia kwenye taratibu za klabu kwa taratibu zilizopo. Baada ya kufanya marekebisho hayo, ndiyo kile kilichokusudiwa ndani ya klabu/vilabu vyenu kitakuwa kimepata baraka za serikali kwa mujibu wa sheria.
Katibu mkuu wa BMT Mohamed Kiganja alisema; "Mabadiliko ya kiundeshwaji wa klabu hizi kongwe ni mazuri na hatuna shida nayo ila sasa je katiba zao wanazifuata na pia wanachama wanashirikishwa kwani inaoonekana kila kitu kinafanyika hapa Dar es Salaam wakati wanachama wako nchini nzima.
"Hizi timu zina mashabiki wengi sana kwahiyo tunajitahidi kutoa elimu kuelekea mabadiliko wanayoendelea ili isije kutokea migogoro ambayo inaweza kuepukika mapema," alisema Kiganja.
No comments:
Post a Comment