Friday, April 14, 2017

TANGAZO


mtandao wa Nacte utafunguliwa kuanzia tarehe 26/4/2017 hadi mwezi wa saba na masomo yataanza mwezi wa tisa mwaka 2017 kwa kozi za

1.TECHNICIAN CERTIFICATE IN PHARMACEUTICAL TECHNOLOGY
sifa za mwombaji
*awe amehitimu kidato cha 4 au 6 na kufaulu masomo manne physics, chemistry, biology na somo lolote la arts(sanaa)

2.BASIC TECHNICIAN CERTIFICATE IN PHARMACEUTICAL TECHNOLOGY
sifa za mwombaji
* awe amehitimu kidato cha 4 au 6 na kufaulu masomo manne ikiwemo chemistry na biology

3.BASIC TECHNICIAN CERTIFICATE IN COMMUNITY HEALTH
sifa za mwombaji
*awe amehitimu kidato cha 4 au 6 na kufaulu masomo manne ikiwemo biology.

Karibu ujiunge na Chuo cha NJOMBE HEALTH TRAINING INSTITUTE. gharama zetu ni nafuu Sana wote mnakaribishwa kwa Mawasiliano zaidi piga simu namba:
0755892807
0755302727
0626414913

Wednesday, March 1, 2017

NGOMA AWAAMBIE UKWELI YANGA ASIUME MANENO.


Na Dr Haroun Haroun.

Yanga  ina  daktari wa  timu  anaitwa  Dr Edward bavu nafikiria  ana  taaluma  ya  kutibia  wachezaj  vizuri, lakini  wakati  mwingine kwa sisi madaktari ikitokea ukishindwa kumtibu mgonjwa unaweza kuomba  daktari  mwenzio akusaidie.

Nilipigiwa  simu  na  Mjumbe  mmoja  wa  yanga ili  nimsaidie  kumtibu Donald Ngoma baada ya kutoka Zanzibar , Nilifanya  hivyo  nafikiria  hii inatokana  na weledi wangu mzuri  wa  uelewa  katika  taaluma  ya  matibabu  ya  michezo, nilimpokea nikamfanyia vipimo pamoja na matibabu (angalia picha na maelezo ya tiba hapo chini).

Nimewasaidia  wachezaji  wa  yanga  waliokuwa  na  shida  mbalimbali za kimatibabu hasa  yale  yaliyokuwa  sugu  katika  michezo (Hissan) wewe ni shahidi, nina  reference  ya Mwashiuya, Juma  Abdul  na Canavaro pamoja na  wachezaj  wengine  mbalimbali  sijawahi  lalamikiwa  hata  siku  moja.

Nilimtibu  Kwa  muda  wa  wiki  mbili  kwa  jeraha la goti  na  kupona  kabisa ,nakumbuka  tarehe  3 Februari,  Yanga  walicheza dhidi ya Stand United  nikiwa nyumbani naangalia mchezo huo ambao Ngoma aliumia na kushindwa kuendelea na mchezo, baadaye nikamwandikia sms kwa  Whatsap  kujiridhisha  kama  bado  jereha  linamsumbua,? akasema, hapana  anachoumwa  Sasa  ni  groin  ikiwa  na maana  kiuno  au  wengine  hupenda  kusema  nyonga na alinijibu Kwa  whatsap  SMS (screen shot nimekutumia), nikamuahidi  kumsaidia  tena  kwa  tatizo  hilo,baada ya matibabu akasema  anajisikia  amepona  na  hata  majibu  ya  vipimo  hayakuonyesha tatizo (picha za vipimo na matibabu hizo nimetuma).

Kitaalamu  Kuna  aina  nne  ya  matibabu  katika  mpira, kuna  sports medicine doctor, physiotherapy, sport nutrition advisor na  chiropractor  ambayo  tunaita  matibabu  mkandamizo  utaalam  huu  nchi  yetu  Hakuna, Ngoma  aliwaongopea  viongozi  wa  Yanga SC  kwa  kuja  na  report  ya  kutengenezwa  kutoka  London  Health  ambayo  imeandikwa  na  physiotherapy  na  siyo  daktari  wa  Michezo.

Fomu  ya  FIFA  ina  sehemu ya daktari  wa  timu na  daktari wa viungo, daktari  wa  viungo  hawez  kuandika  report  Ya  Mchezaji  itakuwa  mara  ya  kwanza  Tanzania.

Ukitazama  report  ya  London  Health  haiko  kwenye maandishi  ya  kidaktari  kabisa inaonekana ilikuwa  mahitaji  ya  Mgonjwa, report  ya  Medical  ina  sehemu  tatu, historia  ya  mgonjwa  ,vipimo  na  ugonjwa  ulioonekana  na  matibabu  yaliyofanyika ambapo daktari  wa  mazoezi  atachukua  report  kutoka  Kwa  daktari.

Niliwaambia ukweli viongozi wa Yanga SC na wewe ukiwemo uliponiuliza (Februari 18) juu ya tatizo lake, nikawajibu kuwa amepona na hana tatizo lolote kiafya hicho ndicho kilichomkasirisha Ngoma na kuamua kunichafua, ukweli ndio umenifanya mimi kuchafuliwa.

Sio kitu  kizuri  kuonyesha  report  ya  Mgonjwa  lakini  hamna  namna, nataka uma wa wana Yanga na wapenzi wa mpira waujue ukweli kuhusu Ngoma, Yanga SC wamekuwa wanaleta  wagonjwa  kwangu  wakati  wana  daktari  wa  timu hii  inaonyesha  ubora  wangu  wa  kazi na imani waliyonayo kwangu, sio jambo jema kwangu kulikalia kimya jambo ambalo linahatarisha mustakabali wa taaluma yangu.

Niwaombe radhi wote niliowakwaza kwa namna moja ama nyingine, nawaomba mliokuwa na imani muendelee kuniamini na sitowaangusha, imani yenu kwangu isipotee kwa jambo hili.

Friday, October 21, 2016

SUALA LA USAJILI WA KESSY, WEKENI KANDO SIASA ZENU BIABIA


Na Saleh Ally

HARUFU ya ushabiki katika suala la kijana Hassan Kessy inazidi kuwa juu kuliko kawaida na wengi wasioelewa, wanaligeuza ni sehemu ya kuonyesha wanaonewa, wananyanyaswa au vinginevyo.

Kessy amejiunga na Yanga akitokea Simba, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ndiyo inayosikiliza kesi hiyo na ilifikia maamuzi kadhaa. Moja ilikuwa ni kumruhusu Kessy kuendelea kucheza kwa ajili ya kuokoa kipaji chake.

Pili ikaamua kuendelea kusikiliza kesi hiyo hadi ilipoipatia uamuzi, tayari ina majibu. Lakini kabla ya kuyatoa, imewataka Simba ambao ni walalamikaji na Yanga ambao ni walalamikiwa kukutana na kulimaliza kirafiki suala hilo.

Wakati hilo linaendelea, juzi Championi Jumatano liliandika kuhusiana na Yanga ambavyo inaweza kupoteza pointi nne kama itashindwa kesi ya Kessy kwa kichwa cha habari kisemacho: “Yanga kupokwa pointi nne”.

Ndani ya ile habari, inaeleza mambo yote ikiwemo Kessy kuruhusiwa kucheza, tahadhari ya Yanga kuacha kumtumia kwa mechi kadhaa na uamuzi wa kamati kuzitaka Yanga na Simba kukutana na kulimaliza suala hilo.

Watu wengi walipiga simu kutaka kupata ufafanuzi, hasa baada ya kumuona Kessy amepangwa katika mechi ya juzi dhidi ya Toto African.

Wengi waliopiga, walionekana husoma lakini hawaelewi, walionekana walisoma mioyo yao ikiwa imezungukwa na mioyo ya hasira ambazo hazina msingi na hawakuelewa, hivyo wakajikuta maswali mengi anayouliza yameelezwa ndani ya habari hiyo.

Wengine ni wale wenye tabia ya kusoma vichwa vya habari na hapo wanaanza kujadili. Habari inaeleza kwa nini Yanga inaweza kupoteza pointi hizo kwa kuwa kesi imeonekana ni ngumu kwao na huo ndiyo ukweli.

Simba sasa nao wanalalamika, kwamba inaonekana TFF wanataka kuipendelea Yanga na ndiyo maana inamchezesha Kessy. Kabla, wako watu wa Simba walipiga kulalamika kwamba kutoa habari ya Kessy ni kuishitua Yanga na hili gazeti ni la Yanga, hivyo tunaitetea kijanja ili isiharibu zaidi.

Ushabiki huu wa hovyo haufai hata kidogo, pia ni vizuri kuacha tukafanya kazi yetu kama chombo cha habari. Watu wanaweza kuwa na ushabiki, waandishi nao ni binadamu, kuna sehemu za kushabikia lakini si kazini au wakati wa kazi.

Suala la Kessy linavyokwenda, utagundua kuna uzembe mwingi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni sehemu kubwa ya uzembe huo, huenda wangetaka kujisafisha, nitakueleza. Wanajua walitoa leseni na wakashughulikia mchakato wa kibali cha Kessy kwenye Shirikisho la Soka Afrika (Caf), bila ya kuangalia mkataba wake na Simba ukoje.

Mwisho kumekuwa na mabadiliko ya mkataba na ule wa chini ya Juni 15, ukaja wa Juni 20, lakini ndani ya Caf, imeshindikana kubadilisha mambo. Huenda TFF ingefurahia kuona inaonekana hakuna kosa, ili isionekane ni sehemu ya kosa.

Simba pia, itafurahia kuona Yanga ina kosa ili ipate nafasi ya kuikomoa Yanga na Kessy, jambo ambalo si jema na si la kimichezo. Hakuna haja ya kuwekeana visasi hata kama Kessy alikosea au Yanga awali walikataa kukaa na Simba.

Kuna figisu, au fitna za kijinga ambazo hazina sababu wala mashiko zinaendelea. Vizuri Yanga na Simba wakaonyesha ukomavu, waliokosewa na Kessy waamini ni kijana wao na wamsadie na kama Simba watafikia hatua ya kusema wanahitaji malipo, basi waangalie si kukomoa ili Yanga walipe na Kessy acheze.

Vitu viko wazi sana, haihitaji kupindishwa au watu kulilia kama wanaonewa sana. Mashabiki wa Yanga au Simba wasiolijua undani wa suala hilo, pia wanapaswa kujifunza na kutuliza akili wakati wanasoma mambo kuliko kuona kulialia au kulalamika sana ndiyo lugha bora ya ufahamu wa mambo.

Sifa za kuonekana unasema sana kijiweni, zinaweza kuwa bora sana kama ukijaribu kuongeza uelewa wa kila jambo unalotaka kulizungumzia. Siasa biabia, (yaani siasa za kubabaisha), hazina nafasi kwenye hali halisi zaidi ni kupoteza muda tu!

Makubaliano ni Mjumbe wa Heshima wa Caf, Said El Maamry awe msuluhishi. Baada ya gazeti hili kutoa habari ya Kessy, ndiyo TFF ikamtafuta na yeye amekubali. Hii ni habari njema kwa Yanga, Simba na Kessy mwenyewe. Itakuwa bora pia El Maamry akipewa heshima na klabu hizo mbili zimtumie kulimaliza suala hilo kwa kuwa pamoja na ufahamu wa juu wa masuala ya Caf, yeye ni mmoja wa wanasheria wakongwe kabisa hapa nchini.

Wakati mwingine vizuri tukijifunza, kama tunataka kufanya mambo bora, vizuri kujifunza au kusikiliza, kusema tu bila ya kujua unachokizungumza, ni hatari kwa matokeo ya baadaye.

Hili suala halishughulikiwi kwa kasi sahihi, TFF ililiacha tu, kuandikwa kumelichangamsha tena. Nisisitize, kama Yanga ikishindwa bado haikwepi kupoteza pointi kama imemtumia beki huyo. 

Hivyo, vizuri TFF ikaliharakisha pia ili Yanga iwe na uhakika zaidi inapomtumia beki huyo, kuliko kumtumia mara kumuacha kama ambavyo imekuwa ikifanya kwa kuwa haikuwa na uhakika.

Omog aweka rekodi mpya Simba


By Dick Dauda -

October 21, 2016

Kocha mkuu wa Simba Joseph Omog ameandika rekodi mpya ndani ya klabu ya Simba msimu huu baada ya kucheza mechi 10 bila kupoteza. Ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Mbao FC kwenye uwanja wa Uhuru, ulikuwa ni ushindi wa nane tangu kuanza kwa msimu huu huku ukiwa ni ushindi wa tatu mfululizo.

Rekodi zinasemaje?

Msimu wa 2009-2010 Patrick Phiri alioongoza Simba kutwaa taji la ligi kuu Tanzania bara bila kupoteza mechi hata moja.

Abdallah Kibadeni ‘King Kibadeni’ akisaidiana na Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ ndiyo makocha wengine walioisaidia Simba kucheza mechi 10 za mwanzo wa ligi bila kupoteza mchezo katika msimu wa 2013-14.

Katika mechi hizo 10 zilizosimamiwa na Kibadeni pamoja na Julio, Simba ilifanikiwa kushinda mechi 5 huku mechi 5 nyingine ikitoka sare. Katika msimu huo, Simba ilipoteza mechi yake kwa mara ya kwanza dhidi ya Azam FC kwa kipigo cha magoli 2-0 msimu ambao pia Azam walitwaa taji la gili mwishoni mwa msimu.

Rekodi aliyoweka Omog

Mcameroon huyo amefanikiwa kuiongoza Simba kushinda mechi nane na kutoka sare mara mbili katika mechi 10 za kwanza tangu kuanzanza kwa msimu huku Simba ikiwa ni timu pekee ambayo bado haijaonja ladha ya kipigo hadi sasa. Licha ya kuwa sawa na King Kibadeni kwa kuiongoza Simba katika mechi 10 bila kupoteza, Omog anabebwa na idadi ya mechi ambazo Simba imepata ushindi.

Simba ikiwa chini ya Omog imeshinda mechi 8 na kutoka sare katika mechi mbili wakati wa Kibadeni Simba ilishinda mechi 5 na kutoka sare katika mechi 5 katika mechi 10 za mwanzoni mwa ligi wakisimama kama wakufunzi wakuu wa klabu hiyo ya mtaa wa Msimbazi.

Je yatajirudia ya msimu wa 2013-14?

Licha ya Simba kuanza vizuri msimu huo, haikufanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi badala yake ikamaliza ligi ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo huku Azam wakitwaa taji hilo kwa mara ya kwanza chini ya Omog aliyerithi mikoba ya Stewart Hall Desemba 2013.

Kwa sasa Simba ipo inaongoza ligi ikiwa chini ya Omog kwa pointi zake 26 baada ya kucheza mechi 10. Omog aliisaidia Azam kutwaa taji la kwanza katika historia yao msimu wa 2013-14. Je msimu huu ataisaidia Simba kutwaa taji la kwanza baada ya kupita kavu katika misimu mitano?

Kutimuliwa

Mwishoni mwa msimu wa 2013-14, King Kibadeni na Julio walifutwa kazi na uongozi wa klabu ya Simba kutokana na klabu hiyo kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi na nafasi hiyo kuchukuliwa na Zdravco Lugarusic.

Licha ya kuwapa ubingwa kwa mara ya kwanza katika historia yao, Azam walimtimua Omog mwaka 2015baada ya kipigo cha magoli 3-0 ugenini na klabu ya El Merreikh ambacho kilipelekea Azam kutupwa nje kwenye ligi ya mabingwa Afrika katika hatua ya awali

Friday, October 14, 2016

MAYANJA AFUNGUKA JUUKO, MAVUGO KUSUGUA BENCHI


Sheila Ally, Mbeya

NYOTA wa Simba, Laudit Mavugo jana alikaa benchi kwa dakika zote 90 akiwaangalia wenzake wanavyopambana kwenye uwanja wa Sokoine dhidi ya Mbeya City na Jackson Mayanja ambaye ni kocha msaidizi ametamka kuwa Simba ni ya wote hivyo watu wasiwe na imani potofu mchezaji anapokaa benchi.

Mayanja aliyazungumza hayo mara baada ya mechi hiyo waliyoshinda bao 2-0 kwamba kitu pekee kilichopo ndani ya Simba kwasasa ni umoja na mshikamano huku akiamini kwamba kila mchezaji ndani ya Simba ana uwezo mkubwa wa kucheza kwa mafanikio.

Mayanja alisema kuwa mechi bado nyingi ambapo wachezaji wote watacheza na si kwamba wanaokaa kwenye benchi uwezo wao umeshuka ila hayo ni mabadiliko ambayo kila mmoja anapaswa kuyaelewa.

"Hata huyo Juuko ana uwezo mkubwa ila watu watofautishe kati ya ngazi ya Taifa na ngazi ya klabu, kwenye klabu ni kugumu kuliko timu ya Taifa hivyo muda utafika hata huku atacheza tu ndio maana nasema Simba ni ya watu wote kila mchezaji anapaswa kuichezea," alisema Mayanja.

Akizungumzia zaidi mechi hiyo alisema kuwa Mbeya City ni timu nzuri ingawa imeshindwa kupata matokeo mazuri huku akifafanua kuwa wao walijiandaa vyema na ndiyo maana wakashinda.

"Ukijipanga vizuri lazima upate matokeo mazuri sisi tulijipanga kuliko Mbeya City, nawapongeza vijana wangu wamecheza kwa kujitolea maana kucheza ugenini ni kugumu, lengo letu tunataka kumaliza mzunguko wa kwanza tukiwa juu kabisa nikiwa na maana kwamba tunataka kufunga hesabu mapema," alisema Mayanja.

Kwa upande wa Mbeya City, kocha Kinnah Phiri alisema kuwa; ,"Tumejitahidi kucheza lakini hatukuwa na bahati na wachezaji wangu walishindwa kutumia nafasi walizopata kama ilivyokuwa kwa wapinzani wetu walipata nafasi wakazitumia vizuri."

Saturday, October 8, 2016

YANGA YETU YAPIGWA CHINI NA SERIKALI

HIVI karibuni Baraza la Udhamini la Yanga lilitangaza kuingia mkataba wa kumkodisha timu Mwenyekiti wao Yusuf Manji kama alivyowaeleza wanachama wake kwenye mkutano mkuu uliopita lakini leo Baraza la Michezo nchini (BMT) limeibuka na kutoa angalizo kwa klabu kongwe hapa nchini kufuatia mabadiliko yanayofanywa ya mfumo wa uendeshwaji wa klabu.

Tayari Yanga kupitia Baraza la Udhamini ilisaini mkataba wa ukodishwaji wa timu, nembo na jengo kwa miaka kumi na Kampuni ya Yanga Yetu Limited, ambapo kauli ya BMT imekuja ikiwa tayari Yanga wamekubali kukodisha mali zake.

BMT imetaja mambo matano ambayo klabu hizo zinapaswa kuyazingia ambayo ni kutumia vikao  mbalimbali ndani ya klabu zao vilivyowekwa kwa mujibu wa katiba zao. Kikao cha kwanza ni kamati ya utendaji  ya klabu. Kamati ambayo itajadili jambo linalokusudiwa kwa kina, kwa kuchambua faida na hasara  ya jambo lenyewe. 

Na wakikubaliana kukubaliana au wakikubaliana kutokukubaliana, muhtasari uandikwe ili upelekwe kwenye kikao cha juu cha klabu  husika. Taratibu za kuitisha kamati ya utendaji zipo kwenye Katiba ya kila klabu na dosari yoyote ikianzia hapa basi zoezi zima litakuwa batili.

Pili, Mkutano Mkuu wa wanachama wote, aidha uwe wa dharula  au wa kawaida, uitishwe na maelekezo ya namna ya kuitisha, kujadiliana na kufikia maamuzi yapo wazi kwenye katiba za klabu. Ni Haki  ya msingi ya wanachama  kupewa taarifa, kuijadili na pengine kuomba ushauri wa kitaalamu au wa kiufafanuzi wapewe pasipo na shaka ili waelewe vizuri, watakapotoa  maamuzi yasiwe na mashaka juu ya haki zao za kikatiba. 


Tatu, Baraza la wadhamini lenye uwezo wa kuingia katika maamuzi makubwa kama haya ni lazima lenyewe liwe lile  lililopitishwa na mkutano mkuu na wala lisiwe la muda. (Baraza la wadhamini la muda). Ikumbukwe kuwa maamuzi haya sio madogo ni maamuzi yanayoweza kusababisha fujo, vurugu, kutokubaliana kwa lolote kutasababisha upotevu/uvunjifu  wa amani si michezo pekee bali nchi kwa ujumla wake.

Nne, Baada ya taratibu hizo zote  kufuatwa muhtasari utaandikwa na kupelekwa kwa msajili ili  kwa mujibu wa sheria ya Baraza ya mwaka 1967 – Kifungu namba 11 (1) kinaeleza 'Chama chochote kinachofanya mabadiliko ya jina, anuani, madhumuni au kifungu chochocte cha katiba yake kitatakiwa kupata idhini ya msajili kwa kupeleka maombi kwa msajili kupitia Msajili  Msaidizi'.
 
Kifungu namba 11 (3) Msajili kuyakataa maombi ya kubadili kifungu chochote cha katiba ya chama kama:- 
a. Ataona kuwa mabadiliko yanaweza kuhatarisha usalama na kuvuruga amani miongoni mwa wanachama na jamii kwa ujumla hivyo kuathiri maendeleo ya chama. 
b.Msajili atabaini kuwa malengo hayo yanalenga kuwanufaisha wachache.
d.Kama anaona kuwa mabadiliko hayazingatii Sera ya michezo na Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa. Msajili ndiyo atatoa  maamuzi  ya kukubali au kukataa kadri  atakavyoona jambo lenyewe kama lina  maslahi kwa nchi au halina.

Mwisho baada ya hatua zote hizo kukamilika, inabidi kufanya marekebisho ya Katiba ambayo yatapitia kwenye taratibu za klabu kwa taratibu zilizopo. Baada ya kufanya marekebisho hayo, ndiyo kile kilichokusudiwa  ndani ya klabu/vilabu vyenu kitakuwa kimepata baraka  za  serikali kwa mujibu wa sheria.

Katibu mkuu wa BMT Mohamed Kiganja alisema; "Mabadiliko ya kiundeshwaji wa klabu hizi kongwe ni mazuri na hatuna shida nayo ila sasa je katiba zao wanazifuata na pia wanachama wanashirikishwa kwani inaoonekana kila kitu kinafanyika hapa Dar es Salaam wakati wanachama wako nchini nzima.

"Hizi timu zina mashabiki wengi sana kwahiyo tunajitahidi kutoa elimu kuelekea mabadiliko wanayoendelea ili isije kutokea migogoro ambayo inaweza kuepukika mapema," alisema Kiganja.


SPS YAMPONGEZA DR COSMAS KAPINGA

TAARIFA YA PONGEZI.
Mnamo tarehe 06.10.2016 majira ya asubuhi,klabu ya Simba kwa kupitia Msemaji wake Ndg Haji Manara ilitangaza Kamati mpya ya Mashindano.Kamati ambayo itakuwa na jukumu kubwa la kuhakikisha Simba SC inapata mafanikio na kutwaa mataji ya Ligi Kuu Tanzania Bara,Kombe la FA,pamoja na mashindano yote ambayo timu yetu itashiriki.
Katika majina yaliyotajwa,sisi wana SIMBA PLATINUM SUPPORTERS tulisikia jina la mmoja wa wadau wetu ambaye ni Makamo Mwenyekiti wa Tawi hili la SPS na daktari mstaafu wa klabu yetu ya Simba Daktari Cosmas Kapinga
Kutajwa kwa Dk Cosmas Kapinga kama mmoja wa wajumbe wa Kamati Mpya ya Mashindano ni FARAJA kubwa kwa Tawi la SpS na hii inatokana na sisi kuamini uwezo wake ktk masuala mazima ya mchezo wa mpira wa miguu.
Tunamuhakikishia Dokta Cosmas Kapinga kuwa TUTAKUWA NAYE BEGA KWA BEGA kwa kila jambo lolote lenye kuonesha umuhimu kwa maslahi ya Simba SC na wana Simba kwa ujumla.
SPS kama Tawi la Simba,inajivunia kuwa na mpambanaji makini na mwenye rekodi safi ndani ya klabu yetu.Tunasema hivyo kwa kuwa tunamfahamu vema Dokta Kapinga.
Pamoja na hayo,tunawapongeza wote waliochaguliwa kama wajumbe wa Kamati hiyo ya Mashindano na Uongozi wa Simba kwa ujumla.
Tunahitaji mataji mbalimbali ndani ya Simba kwa sasa.
Kila la heri kwa Simba SC
Mungu tubariki wana Simba SC.
IMETOLEWA NA TINGA NAMBA MOJA LA MICHEZO -SPS.

Like
Co