Na Tausi Salum
DUAza Watanzania zielekezwe pia kwa timu ya Taifa ya Mpira
wa Miguu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti
Boys’, iliyoondoka leo saa 12.00 Uwanja wa Ndege ya Mwalimu
Julius K. Nyerere, Dar es Salaam, Tanzania kwenda Antananarivo,
Madagascar kupitia Uwanja wa Ndege wa Ndege ya Oliver Tambo
jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Alfred Lucas, alisema Serengeti Boys inayokwenda kuweka kambi
huko Antananarivo, Madagascar inatarajiwa kufika huko saa 8.10
mchana. Timu hiyo inajiandaa kucheza na Afrika Kusini katika
mchezo wa awali kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la
Mataifa ya Afrika utakaofanyika Agosti 6, 2016.
Alisema mchezo wa marudiano utafanyika Agosti 21, mwaka huu
kwenye Uwanja wa Azam, ulioko Chamazi-Mbagala, nje kidogo ya
jiji la Dar es Salaam. Serengeti ipo kwenye ushindani wa kuwania
nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana,
zitakazofanyika mwakani huko Madagascar.
Wakati mkuu wa msafara akiwa ni Ayoub Shaibu Nyenzi ambaye
ni Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Vijana, maofisa wengine
waliosafiri na timu hiyo ni Kocha Mkuu, Bakari Nyundo Shime,
Daktari wa timu hiyo, Shecky Francis Mngazija na Mtunza Vifaa,
Andrew Vanance Andrew pamoja na Juma Kaseja Juma ambaye
kwa muda amechukua nafasi ya makocha wasaidizi, Sebastian
Nkoma na Muharam Mohammed ‘Shilton’ wanaohudhuria kozi ya
makocha ngazi ya juu inayoratibiwa na CAF.
Nyota waliosafiri ni pamoja na makipa, Ramadhani Awm Kabwili,
Kelvin Deogratius Kayego na Samwel Edward Brazio wakati
mabeki wako Kibwana Ally Shomari, Nickson Clement Kibabage,
Israel Patrick Mwenda, Dickson Nickson Job, Ally Hussein
Msengi, Issa Abdi Makamba na Enrick Vitalis Nkosi.
Viungo ni Kelvin Nashon Naftal, Ally Hamisi Ng’anzi, Asadi Ali
Juma Ali, Syprian Benedictor Mtesigwa, Ibrahim Abdallah Ali,
Shaban Zuberi Ada huku washambuliaji wakiwa ni Mohammed
Abdallah Rashid, Yohana Oscar Mkomola na Muhsin Malima
Makame.
“Najua mchezo utakuwa mgumu, lakini nakiamini kikosi change.
Kiko imara,” amesema Shime, maarufu zaidi kwa jina la Mchawi
Mweusi.
Serengeti Boys inakwenda kucheza na Afrika Kusini baada ya
kuwatoa Shelisheli kwa jumla ya mabao 9-0 katika mechi zake
mbili za kimataifa. Mshindi wa jumla kati ya Serengeti Boys na
Afrika Kusini, atacheza na timu mshindi kati ya Namibia na
Congo-Brazaville.
Hivi karibuni Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako
walishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na
FIFA (AIFF International Youth Tournament 2016) kabla ya
kurudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu katika Tanzania na kwa
nchi za Afrika Mashariki. Ilishika nafasi ya tutu nyuma ya Korea
Kusini na Marekani.
mwisho